Rwanda na Tanzania zimetoshana nguvu baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana kwenye mchezo wa Kimataifa wa kirafiki uliopigwa uwanja wa Amahoro huko Rwanda
Ulikuwa ni mchezo muhimu ambao matokeo ya ushindi kwa timu zote yangenufaisha viwango vya FIFA kwani ni mchezo uliokuwa kwenye kalenda ya FIFA
Rwanda ilitengeneza nafasi chache za wazi kwenye kipindi cha kwanza lakini washambuliaji wake Meddie Kagere na Jacques Tuyisenge walishindwakuzitumia
Katika kipindi cha pili Rwanda ikimtumia kiungo Haruna Niyonzima ambaye alikuwa nahodha wa timu hiyo leo, ilitengeneza nafasi zaidi lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Stars iliyokuwa chini ya nahodha Erasto Nyoni na Bakari Mwamnyeto pamoja na mlinda lango Metacha Mnata, waliweza kuokoa mashambulizi kadhaa huku nafasi nyingine wakipoteza Rwanda wenyewe kutokana na kukosa umakini langoni
Pamoja na kutengeneza nafasi chache, bado safu ya ushambuliaji ya Stars haikuonyesha kuwa na makali ya kuweza kufunga kwenye mchezo huo
Ni dhahiri Kaimu Kocha Mkuu Etienne Ndayiragije anapaswa kuifanyia kazi safu hiyo kuelekea mchezo wa CHAN dhidi ya Sudan utakaopigwa Uganda Oktoba 18
Stars inahitaji kushinda kuanzia mabao mawili ili kukata tiketi ya kucheza fainali za michuano ya CHAN mwakani