Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba Swedi Mkwabi amesema amejiondoa katika nafasi hiyo ili kuondoa mgogoro uliokuwa ukifukuta na hivyo kuipa nafasi Simba kujikita zaidi kwenye masuala ya maendeleo
Mkwabi amejiondoa kutokana na sintofahamu iliyojitokeza baina yake na Mwekezaji wa Simba Bilionea Mohammed Dewji 'Mo'
Baada ya kuwa kimya tangu ajiuzulu, Mkwabi amesema kujiondoa kwake kulikuwa na lengo zuri la kunusuru maendeleo ya klabu hiyo
Hata hivyo Mkwabi amesema kuna mambo yamsingi yanapaswa kufanyiwa mabadiliko haraka ndani ya uongozi wa Simba
"Naamini nimefanya uamuzi wa busara na wa kishuja kukaa pembeni Simba, huu sio wakati wa klabu kufikiria masuala ya ugomvi badala ya maendeleo, hivyo ili wasifikirie ugomvi zaidi na kusahau maendeleo, nimeona nifanye busara kukaa kando," Mkwabi aliliambia gazeti la Mwanaspoti
"Ingawa kinachoendelea ndani ya klabu ya Simba kwa sasa kama hakutakuwa na mabadiliko, basi muda ndiyo utazungumza na ukweli utajulika siku si nyingi"
Hata hivyo, Mkwabi licha ya kujiuzulu amesema muda aliodumu madarakani Simba, anajivunia mambo makubwa manne aliyoshiriki kikamilifu kuyafanya na yatabaki kuwa alama kwenye uongozi wake.
"Kikubwa ninachojivunia ni kuwa miongoni mwa walioiongoza Simba kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita pamoja na kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo"
Hata hivyo, alisema licha ya mafanikio hayo, jambo kubwa lililomkwaza kwenye uongozi wake katika kipindi chote akiwa Mwenyekiti wa Simba ni unafiki wa baadhi ya viongozi.
"Unafiki katika mpira upo sana, simaanishi katika Bodi ya Wakurugenzi pekee, lakini nazungumzia βgeneralβ unafiki ni jambo ambalo limenikwaza kipindi cha uongozi wangu na nitaendelea kulichukia"
Alisema katika uongozi wake alipenda zaidi ukweli na uwazi kwenye mambo yanayohusu klabu, lakini alichojifunza katika mpira, mtu mkweli na anayesimamia masilahi ya wengi huwa hapendwi.
Hata hivyo, Mkwabi alisema hajafikiria kama miaka ijayo atarudi kugombea ili kuongoza klabu hiyo ambayo baada ya kujiuzulu anaendelea kuitumikia kama mwanachama wa kawaida.
Baada ya Mkwabi kuachia wadhifa huo, kumekuwa na taarifa aliyekuwa Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah (Try Again) amekuwa akitajwa kurithi nafasi hiyo.
Taarifa kutoka mitaa ya Msimbazi, zinaeleza Try Again ambaye aliiongoza Simba kuingia kwenye mfumo wa mabadiliko, amekuwa akishawishiwa na baadhi ya wanachama na wengine wakiahidi kumchukulia fomu muda ukifika.
Hata hivyo, mwenyewe amesema kwa sasa hana mpango huo
Mkwabi aliingia katika mvutano na Mo akidaiwa kushinikiza mwekezaji huyo aweke Bilioni 20 kwenye akaunti ya klabu
cutMara kadhaa Mkwabi alidaiwa kutounga mkono Mo kuendelea kutumia fedha zake za mfukoni kuiendesha Simba akihofia baadae Simba inaweza isinufaike na uwekezaji wake
Kumekuwa na taarifa ambazo hazijathibitishwa na uongozi kuwa Mo amekuwa akiikopesha Simba fedha ambazo klabu haina uwezo wa kuzilipa na pengine zitakatwa katika fedha za uwekezaji
Upande wa Mo yeye alikuwa akimtuhumu Mkwabi kuihujumu klabu kwa kushirikiana na Mzee Hamisi Kilomoni na kundi lake
Mo aliamini hata suala la kupatikana kwa hati ya Simba lilikuwa likikwamishwa na Mkwabi