Mshambuliaji wa zamani wa Simba Mussa Mgosi ambaye ni kocha wa Simba Queens amesema mshambuliaji mpya wa timu hiyo raia wa Brazil Wilker Da Silva ni moto wa kuotea mbali
Wilker amerejea kikosini hivi karibuni baada ya kuwa nje kwa zaidi ya wiki tano akisumbuliwa na majeruhi
Jana alishiriki mchezo wa kirafiki kati ya Simba dhidi ya Azam B, akifunga moja ya mabao ya Simba kwenye ushindi wa mabao 3-0
Bado mashabiki wa Simba hawajamuona mshambuliaji huyo akiwa dimbani hali iliyopelekea wengine kuanza kuhoji uwezo wake
Mgosi amewatoa hofu mashabiki hao kwa kuwaambia Wilker ni 'bonge la mshambuliaji'
"Wilker nimekuwa nikimsikia tu tangu amekuja, jana niliposikia wana mechi na yeye atakuwepo, niliona nifike uwanjani kumuangalia"
"kwa nilivyomuona ni straika mzuri, ana vitu vingi, atakuwa msaada mkubwa kwa Simba," amesema
"Kwa hao wanaowasema sijui walitaka Simba ilete Wabrazil kama walivyokuwa kina Gaucho, Neymar, Ronaldo… hata sijui wanachokitaka kwa sababu huyu mchezaji ana kiwango cha kucheza Simba"
"Japo nimemuona kwa muda mfupi na ametoka katika majeraha, ila kwa vitu alivyoonyesha, inaonyesha wazi ni mchezaji atakayekuja kufanya mambo makubwa"
Wilker amerejea kikosini wakati muafaka kwani washambuliaji tegemeo John Bocco na Meddie Kagere ni majeruhi