Mbrazili Gerson Fraga ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao akimtungua kipa Aishi Manula katika mazoezi ya Simba leo Jumatatu Septemba 16, 2021.
Kiungo huyo mkabaji Mbrazili ameng'aa katika mazoezi ya leo yanayofanyika kwenye Uwanja wa Gymkhana baada ya kuongoza kufunga mabao ya kideo.
Fraga amemfunga Manula mabao matatu mazuri huku kiungo mwingine Clatous Chama akifunga moja.
Kocha wa Simba Patrick, Aussems aligawa vikosi viwili ambavyo vilicheza kama mechi kimoja kilikuwa na Chama, Fraga, Said Ndemla, Pascal Wawa, Fransis Kahata ambacho kipa wao alikuwa Beno Kakolanya na kingine kiliongozwa na Gadiel Michael, Shomari Kapombe, Yusuph Mlipili, Aharif Shoboub, Ibrahim Ajib na kipa Manula.
Katika mazoezi hayo Fraga alionekana kuwa na kasi akipiga chenga maridadi na kufunga mabao mazuri.
Kati ya mabao matatu aliyofunga mchezaji huyo mawili aliyafunga kwa shuti na kumuacha Manula asijue la kufanya.
Jambo hilo lilisababisha wenzake kumtania kwa kusema alipolala leo alale kila siku ikiwemo siku za mechi za Ligi ili aendelee kufunga.
Licha ya Fraga kuanza katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara msimu huu dhidi ya JKT Tanzania na Mtibwa Sugar, lakini bado hajawashawishi mashabiki wa klabu hiyo kutokana na aina ya uchezaji wake wa taratibu huku akipenda kupiga pasi za pembeni na kushindwa kuipeleka timu mbele kushambulia.
Mchezaji huyo alianza katika michezo hiyo na kumuweka nje Jonas Mkude.