Mzamiru Yassin, kiungo kiraka wa Simba, ametajwa kuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi hicho, ambao hufanya kazi kubwa kusaidia ushindi
Kocha Mkuu wa mabingwa hao wa Tanzania Bara, Patrick Aussems amesema kiungo huyo amekuwa akitimiza wajibu wake kikamilifu katika michezo anayopewa nafasi
Amfananisha na mashine
Aussems amesema Mzamiru hupata pointi nyingi katika kila mechi anayocheza na kwake anamfananisha na "mashine" muhimu katika kikosi chake.
"Ni mchezaji mzuri, hufuata maelekezo na hucheza kwa hesabu, anajua kucheza katika eneo lake, kwa kumuangalia kiufundi, nasema ni mchezaji muhimu"
Pia amemtaja ni mchezaji anayependa kufanya mazoezi wakati wote na ushindani wa kuwania namba katika kikosi cha kwanza umesaidia kumuimarisha.
"Kila mmoja anapenda kuwapo katika kikosi cha kwanza, na kama upo, utaona hakuna mchezaji anayezembea kwa sababu hawataki kuona wanaanzia benchi, kurudi katika kikosi hicho huitaji nguvu ya ziada, kwa kifupi nafurahishwa naye na kazi anayoifanya"
Mzamiru ameanza msimu vyema akitengeneza mabao mawili ya Simba yaliyofungwa na Meddie Kagere kwenye ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya JKT Tanzania