Kiungo wa kimataifa wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutoka Sudan, Sharaf Eldin Shiboub, amesema kuwa akili na mawazo yao yote ni kupambana ili kuhakikisha wanashinda taji la ligi hiyo kwa mara ya tatu mfululizo.
Kiungo huyo fundi amesema Simba ina kila sababu ya kushinda ubingwa wa ligi kuu hasa baada ya kutolewa kwenye mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika
Shiboub raia wa Sudan amesema kuwa watahakikisha wanashinda kila mechi kwa sababu wanataka kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea taji hilo na hatimaye kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa hapo mwakani.
"Malengo yetu ni kushinda mechi zetu zote, tumeongeza nguvu kwenye ligi, tunahitaji kufanya vizuri zaidi, tumejipanga na ninaamini tutafanikiwa," alisema Shiboub, kiungo huyo wa Timu ya Taifa ya Sudan.
Aliongeza kwamba hasira ya kutolewa mapema katika mashindano ya kimataifa, ndiyo inawafanya wajiweke tayari kushinda mechi za Ligi Kuu na kuwapa furaha mashabiki wa timu yao.
Simba ambayo ilianza kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya JKT Tanzania, itaikaribisha Mtibwa Sugar katika mchezo wa raundi ya pili ya Ligi Kuu Bara utakaochezwa Septemba 17 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.