Uongozi wa klabu ya Simba umepokea barua kutoka Wydad Casablanca inayotaka kumsajili beki wa timu hiyo Juuko Murshid
Mtendaji Mkuu wa Simba Crescentius Magori amesema wamefikia makubaliano kumuachia Juuko ajiunge na timu hiyo baada ya Wydad kukubali kununua mkataba wake na Simba
Magori amesema mkataba wa Juuko na Simba ulipaswa kumalizika mwezi Novemba, Wydad wamekubali kununua muda uliobaki
"Tumekubaliana na Wydad juu ya usajili wa Juuko. Wamekubali kununua muda wa mkataba uliobaki hivyo tutawapa barua ya kumuachia," amesema
Juuko alikuwa na mgogoro na uongozi wa Simba baada ya kuondoka kambini mwishoni mwa msimu uliopita bila ya ruhusa ya uongozi
Aidha mchezaji huyo hakurudi nchini kujiunga na kambi Afrika Kusini, licha ya uongozi kumuandikia barua mara kadhaa
Uamuzi wake wa kuondoka kambini kinyemela ulipelekea Simba kusitisha kumlipa mshahara