Serikali imefafanua kuwa Sheria ya uwekezaji kwenye vilabu vya soka nchini iliyoruhusu wawekezaji kupewa hisa asilimia 49 na Wanachama asilimia 51, imetamka kuwa wawekezaji ni lazima wawe zaidi ya mmoja
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Waziri wa habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe amesema sheria hiyo inataka wawekezaji waanzie watatu na kuendelea
Waziri Mwakyembe amesema Sheria hiyo haikusimamiwa ipasavyo na TFF hivyo Serikali imeanza mchakato wa kutunga kanuni na marekebisho ambapo zoezi hilo litasimamiwa na BMT
"Hairuhusiwi mwekezaji mmoja kuhodhi asilimia 49, mchakato ulipoanza tuliwambia TFF wasimamie ipasavyo, lakini hawakufanya hivyo," Dk Mwakyembe aliwaambia waandishi wa habari
"Hivyo tumeanza mchakato wa kanuni ya marekebisho na mchakato huo utafanya na BMT na si TFF"
Simba imekuwa klabu ya kwanza kufanya maadiliko ya mfumo wa uendeshaji ambapo hata hivyo huenda ikalazimika kufanya mabadiliko kidogo ili kukidhi matakwa hayo ya Sheria
Kwa sasa mwekezaji wa Simba Bilionea Mohammed Dewji 'Mo' amenunua hisa asilimia 49 peke yake