Kama msimu uliopita kwenye ligi timu ziliusaka mpira 'kwa tochi' dhidi ya Simba, basi msimu huu hali hiyo inaweza kuwa mara dufu baada ya mabingwa hao wa Tanzania Bara kuongeza mafundi kwenye kikosi
Katika siku yake ya kwanza mazoezini huko Afrika Kusini, kiungo Francis Kahata alidhihirisha kwa nini alistahili kusajiliwa na Simba baada ya kuonyesha uwezo mkubwa wa kupiga pasi za uhakika
Katika mazoezi hayo Kahata pengine ndiye mchezaji aliyepiga pasi nyingi zaidi
Wakati Kahata akifanya yake, mzee wa 'makorokoro' Ibrahim Ajib na fundi Clatous Chama nao hawakuwa nyuma
Watatu hawa wanatabiriwa kutengeneza utatu wa hatari kwenye safu ya kiungo
Akizungumzia siku mbili za mazoezi ya kikosi chake, kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wachezaji wake wameweza kufuata kile anachowaelekeza
Amekiri ujio wa nyota wapya utaiongezea timu hiyo makali kuliko msimu uliopita
Simba inatarajiwa kucheza mchezo wake wa kwanza wa kirafiki huko Afrika Kusini Jumatano ijayo, Julai 23 2019