Hakuna shaka msimu ujao furaha itaendelea kutamalaki Msimbazi kutokana na usajili makini uliofanywa na mabingwa hao wa nchi
Simba imefanya usajili makini ambao kwa hakika unaweza kutimiza ndoto za timu hiyo kunyakua taji la ligi ya mabingwa Barani Afrika
Ndio! moja ya malengo ya msimu unaokuja ni kufanya vizuri kwenye michuano ya ligi ya mabingwa, hesabu ikiwa kuvuka hatua ya robo fainali
Achana na maboresho yaliyofanywa kwenye safu ya ulinzi, Simba imefanya maboresho katika safu ya kiungo na ushambuliaji
Ibrahim Ajib na Francis Kahata wametua kuiongezea Simba ubora katika kutengeneza mabao

Msimu uliopita Ajib alitoa pasi 17 za mabao na mwenyewe kufunga mabao sita wakati Kahata amekuwa akiifanya kazi hiyo katika klabu ya Gor Mahia kwa misimu kadhaa
Mshambuliaji Meddie Kagere amefurahia ujio wa Kahata Simba kwa kuwa ni mchezaji ambaye alikuwa akiifanya kazi yake ya kufumania nyavu kuwa nyepesi wakati akiwa Gor Mahia
Mafundi hao wanakuja kuungana na Clatous Chama ambaye msimu uliopita alikuwa 'engine' ya safu ya kiungo akishirikiana na Jonas Mkude na James Kotei aliyetimkia Kaizer Chiefs
Simba hii ni hatari, msimu ujao unaweza kuwa mgumu kwa timu za ligi kuu zitakapokutana na mnyama pengine kuliko msimu uliopita