Kiwango alichoonyesha mshambuliaji Emmanuel Okwi kwenye michuano ya Afcon, kimebadili upepo Msimbazi ambapo inaelezwa juhudi zinafanyika kumbakisha mkali huyo wa kuzifumania nyavu
Juzi Okwi aliiongoza Uganda kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya DR Congo yeye akifunga bao moja pia akiibuka mchezaji bora wa mchezo huo
Okwi aliondoka Simba kujiunga na kambi ya timu ya Taifa ya Uganda bila ya kusaini mkataba licha ya kufanya mazungumzo na mabosi wa usajili
Mkataba wake umemalizika hivyo yuko huru
Inaelezwa uongozi wa Simba uko tayari kumtimizia mahitaji yake ili aweze kubaki Msimbazi lakini changamoto iliyoko sasa ni mchezaji huyo kupanda thamani baada ya kuanza vyema michuano ya Afcon
Inaelezwa timu nyingi zinapigana vikumbo kuiwania sahihi yake baada ya kun'gara mchezo dhidi ya DR Congo
Juzi baada ya mchezo, Okwi aliwaambia waandishi wa habari kuwa hatma yake itafahamika baada ya michuano ya Afcon kumalizika
Ili kuweza kumtumia kwenye michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao, Simba inapaswa kukamilisha usajili wake kabla ya Jumapili ya wiki hii