Mlinda lango mpya wa Simba Beno Kakolanya amesema hajajiunga na timu hiyo ili kuwa kipa msaidizi
Kakolanya aliyetambulishwa mapema wiki hii, amesema atahakikisha analishawishi benchi la ufundi ili aweze kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza
Kakolanya aliyekuwa kipa wa kutegemewa na Yanga kabla ya kuamua kujiondoa kikosini baada ya timu hiyo kushindwa kumlipa mishahara na fedha zake za usajili, amesema anaheshimu uwezo wa makipa waliopo Simba lakini nae atahakikisha anapata nafasi kikosini
Amewataka wale wanaoamini kujiunga kwake Simba ndio mwisho wake, wasubiri waone
"Naheshimu uwezo wa Manula na Dida lakini kwa nafasi yangu nitaonyesha nilichonacho, sina presha wala nini na nimekuwa nikisikia mengi kuwa huu ndio mwisho wangu nadhani watu hawajui maisha ya mpira yalivyo," amesema
"Nimekuwa na maisha mazuri Yanga na yenye furaha, nadhani umefika muda wa kuangalia mbele ili kukabiliana na maisha mapya"
"Nitashirikiana na Manula pamoja na Dida, naamini tutafanya kazi nzuri msimu ujao"
Ujio wa Kakolanya umezidi kuimarisha nafasi ya langoni na pengine sasa mlinda lango namba moja Aishi Manula atapata muda mwa kupumzishwa baadhi ya michezo kwani amekuwa kipa anayedaka michezo karibu yote ya msimu mzima