Kocha Mkuu wa Simba, mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara, Patrick Aussems ameshangazwa na ratiba iliyopangwa na Bodi ya ligi akieleza inaweza kuathiri afya za wachezaji wake
Aussems ambaye atakiongoza kikosi cha Simba leo kuikabili Coastal Union mkoani Tanga, ameshangazwa Simba kutakiwa kucheza michezo 8 katika kipindi cha siku 19
Mbelgiji huyo aliyefanikiwa kuipeleka Simba robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, amesema ratiba hiyo haikuzingatia muda ambao watatumia kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine
"Tumerejea kwenye ligi kuu na tunapaswa kucheza michezo nane ndani ya siku 19. Tutasafiri Tanga, Bukoba, Mwanza, Musoma, Morogoro na Mbeya. Muda wa kusafiri haukujumuishwa, vipi kuhusu afya za wachezaji?," amehoji Aussems
Kampeni ya Simba ya kumaliza viporo vyake inaanza hii leo, April 17 katika dimba la Mkwakwani ambapo itavaana na wenyeji Coastal Union kabla ya kusafiri hadi Kagera kucheza na Kagera Sugar, April 20.
April 23, Simba itasafiri hadi jijini Mwanza kucheza na Alliance FC kisha April 26 kucheza na KMC.
Tarehe 28 April itasafiri hadi mkoani Mara kucheza na Biashara United kabla ya Mei mosi kucheza na Tanzania Prisons jijini Mbeya.
Ratiba hiyo ya viporo itaendelea tena Mei 5 kwa kucheza na Mbeya City huko huko jijini Mbeya.