Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba kesho wanaelekea jiji la Lubumbashi huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo tayari kwa mchezo wa pili wa robo fainali ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya TP Mazembe
Ili kuepuka hujuma Simba inaifuata TP Mazembe siku moja kabla ya mchezo kwa kutumia usafiri wa Ndege ya kukodi. Mchezo utapigwa Jumamosi April 13 2019 saa kumi kamili jioni
Wekundu hao wa Msimbazi waterejea nchini keshokutwa Jumamosi jioni baada ya mchezo
Baada ya kulazimishwa suluhu ya bila kufungana kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Taifa, kikosi cha Simba kinakwenda DR Congo kikiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema aliridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake kwenye mchezo wa kwanza na anaamini wanao uwezo wa kupata matokeo ugenini na kutinga nusu fainali
"Ingawa hatukupata ushindi kwenye mchezo wa kwanza, tulicheza vizuri sana, tulipoteza nafasi nyingi za wazi ambazo tulitakiwa kufunga," Aussems amewaambia waandishi wa habari kwenye mazoezi ya Simba yanayofanyika uwanja wa Boko Veterans
"Tunajiandaa kikamilifu kwa ajili ya mchezo wa marudiano, nina matumaini tutashinda na kuingia nusu fainali"
"Tumefanyia kazi makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo uliopita, tuko tayari kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano"
Matokeo ya ushindi au sare ya mabao yataihakikishia Simba kutinga nusu fainali ya michuano hiyo na kuandika rekodi nyingine ya kipekee