Kikosi cha mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba tayari kimeelekea mkoani Morogoro kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mbao Fc utakaopigwa kwenye uwanja wa Jamhuri
Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu amesema wameelekea Morogoro wakiwa na matumaini makubwa ya kupata matokeo mazuri dhidi ya Mbao Fc Jumapili
Rweyemamu amesema wanafahamu watachuana na timu ambayo imekuwa na tabia ya 'kuwasumbua' kuanzia msimu uliopita hivyo wameuchukulia mchezo huo kwa umuhimu mkubwa
"Tunaelekea mkoani Morogoro tukiwa na kikosi chetu kamili. Tunawaheshimu Mbao sababu msimu uliopita walitupa changamoto na hata msimu huu pia hatukupata matokeo mazuri katika mchezo wa kwanza," amesema
"Ni imani yetu kutokana na maandalizi tuliyofanya, tutapata matokeo mazuri Jumapili"
"Leo jioni na kesho asubuhi tutafanya mazoezi kwenye uwanja wa Jamhuri, yakiwa ni maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo"
Mbao Fc ndio timu pekee iliyopata ushindi dhidi ya Simba msimu huu ikifanya hivyo katika mchezo wa duru ya kwanza uliopigwa katika dimba la CCm Kirumba
Simba na Mbao Fc pia zilikutana kwenye michuano ya SportPesa katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, mchezo ambao ulimalizika kwa timu hizo kutoka suluhu ya bila kufungana, Simba ikifanikiwa kuibuka na ushindi kupitia changamoto ya mikwaju ya penati
Simba inahitaji kushinda mchezo huo ili kuendelea kuzisogelea Azam Fc na Yanga zilizojuu yake katika msimamo wa ligi