Ushindi wa mabao 2-1 iliyopata Simba juzi dhidi ya AS Vita Club umeongeza morali ya kikosi cha kocha Patrick Aussems kuelekea mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting leo
Wiki hii imekuwa ya shangwe kwa mashabiki wa Simba baada ya kuishuhudia timu yao ikipenya hatua ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika licha ya kutopewa nafasi kubwa awali
Simba imepania kuendeleza wimbi la ushindi katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa katika dimba la Taifa kuanzia saa moja jioni. Katika mchezo wa duru ya kwanza Simba iliifumua Ruvu Shooting mabao 5-0
Licha ya kuwakosa baadhi ya wachezaji walioitwa timu za taifa, kocha msaidizi wa Simba Denis Kitambi amesisitiza wana kikosi kipana
Kitambi amesema malengo ya Simba ni kushinda michezo yote iliyobaki ili kutetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita
"Mikakati yetu ni kushinda mechi zote zilizobaki ili kutetea ubingwa wetu, ushindi dhidi ya Ruvu Shooting utatupa taswira ya kule tunapokwenda," amesema Kitambi
Jana Simba ilifanya mazoezi ya mwisho yaliyosimamiwa na Kitambi, kwenye Uwanja wa Boko Veterans kabla ya mchezo huo wa leo
Katika mazoezi hayo, Simba ilikuwa na wachezaji 18, huku wengine wakipumzishwa na baadhi yao kujiunga na timu zao za taifa zinazojiandaa kwa mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Matifa ya Afrika (AFcon 2019).
Wachezaji wa kimataifa waliokwenda katika timu zao za taifa ni Meddie Kagere (Rwanda), Emmanuel Okwi na Juuko Murushid (Uganda) na Clatous Chama (Zambia).
Wengine ni Aishi Manula, John Bocco, Jonas Mkude na Erasto Nyoni walioitwa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania