Uwanja wa Taifa jana ulifurika hasa! Takwimu zinaonyesha karibu mashabiki elfu 60 waliingia uwanjani kushuhudia mchezo wa ligi ya mabingwa kati ya Simba dhidi ya Vita Club
Huu sasa umekuwa utamaduni kwa mashabiki wa Simba kuujaza uwanja huo kwa michezo 'mikubwa' ambayo Simba inacheza
Utamaduni huu umewaingiza hofu wapinzani wa Simba hasa wanaokuja kucheza katika dimba la Taifa
Katika nchi nyingi barani Afrika imezoeleka viwanja hujaa pale inapocheza timu ya Taifa.
Lakini hali ni tofauti kwa Tanzania ambapo kwa miaka ya hivi karibuni Simba imekuwa ikiujaza uwanja huo tena wakati mwingine kuliko hata ikicheza timu ya Taifa
Pamoja na nguvu kubwa ya uhamasishaji, mashabiki wa Simba wamejitambua na wanafahamu umuhimu wa kwenda uwanjani kuisapoti timu
Matokeo ya ushindi katika dimba la Taifa hasa kwa michezo ya ligi ya mabingwa, yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na motisha ya mashabiki kwa wachezaji
Wingi wa mashabiki unawafanya wachezaji wajihisi kuwa na kazi zaidi ya kufanya na hakika hilo limedhihirika kwa Simba kufanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa