Baada ya kuichapa Stand United mabao 2-0 hapo jana, kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema sasa wanaelekeza nguvu kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya JS Saoura
Mchezo huo utapigwa March 09 nchini Algeria
Akizungumza baada ya mchezo jana, Aussems alisema matokeo waliyopata yamekiweka kikosi chake katika hali nzuri kuelekea mchezo huo muhimu
"Ushindi huu ni muhimu kwetu kwa kipindi hiki ambacho tunajiandaa kwenda kucheza na JS Saoura," alisema Aussems
Kikosi cha Simba kimelala mkoani Mwanza na leo kinatarajiwa kurejea jijini Dar es salaam kujiweka sawa kabla ya safari ya kuelekea Algeria
Simba ina nafasi nzuri ya kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa
Inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi D ikiwa na alama sita nyuma ya vinara Al Ahly wenye alama saba
Matokeo ya ushindi au sare kwenye mchezo dhidi ya JS Saoura yataiweka Simba katika nafasi nzuri zaidi ya kutinga robo fainali kwani mchezo wake wa mwisho ni dhidi ya Vita Club na utapigwa kwenye uwanja wa Taifa
JS Saoura inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama tano wakati Vita Club inaburuza mkia ikiwa na alama nne
Kundi D limekuwa na ushindani mkali ambapo kila timu bado ina nafasi ya kufuzu
Wakati Simba ikiwa ugenini kuikabili JS Saoura, Vita Club itakuwa nyumbani ikipepetana na Al Ahly