Baada ya kuwa na idadi kubwa ya michezo ya viporo, uongozi wa Simba umesema utacheza michezo yake yote ya ligi sambamba na ile ya ligi ya mabingwa bila ya kujali changamoto ya ratiba
Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori amesema kwa sasa timu hiyo inakabiliwa na ratiba ngumu kwenye ligi kutokana na michezo yake kuwa karibukaribu lakini wataitumia michezo hiyo kama sehemu ya maandalizi ya michezo ya ligi ya mabingwa
"Tuna ratiba ngumu ya mechi za karibukaribu katika Ligi Kuu Bara ambazo kwetu tunatakiwa kupata ushindi kwa ajili ya kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi."
"Lakini nje ya kupata pointi kwenye mechi hizo zote, mechi hizo tunazichukulia kama sehemu yetu ya maandalizi kwa ajili ya mechi yetu ya kimataifa dhidi ya JS Saoura," amesema
Baada ya kucheza na Yanga Februari 16, Simba ilielekea mkoani Arusha kuikabili African Lyon Februari 19 na kesho Februari 22 itashuka uwanja wa Taifa kuikabili Azam Fc
February 26 itakuwa mkoani Iringa kuikabili Lipuli Fc na March 03 kuelekea mkoani Shinyanga kuikabili Stand United.
Baada ya mchezo huo Simba itaelekea nchini Algeria kucheza na JS Saoura
Wakati ligi kuu ya Tanzania Bara ikiingia mzunguuko wa 28, Simba imeshuka dimbani mara 17 tu ikiwa na deni la michezo 11
Hivi karibuni Mtendaji wa Bodi ya Ligi Boniface Wambura alisema Simba pamoja na timu nyingine zenye viporo zitalazimika kumaliza viporo hivyo kabla ya ligi kuingia kwenye mzunguuko wa 30