Hakuna anayeweza kubisha kuwa katika ligi ya hapa Tanzania ubora wa Simba umeziacha mbali sana timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo ikiwemo Yanga ambayo mafanikio yao msimu huu yamechangiwa zaidi na bahati
Baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya vigogo wa soka Barani Afrika Al Ahly, Simba itaingia kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Yanga ikiwa na morali kubwa
Aidha matokeo ya ushindi dhidi ya Al Ahly yameongeza hofu kwa wapinzani wao ambapo kocha Mwinyi Zahera atakuwa anajiuliza ni vipi ataweza kuidhibiti timu iliyokiangusha kigogo cha soka barani Afrika siku chache zilizopita?
Katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza timu hizo zilitoka suluhu ya bila kufungana lakini Yanga ilipaswa wamshukuru mlinda lango wake Beno Kakolanya ambaye alikuwa nyota wa mchezo huo
Hata hivyo Kakolanya kwa sasa sio sehemu ya kikosi cha Yanga kitakachoikabili Simba hapo kesho baada ya kuondolewa kikosini na Zahera kufuatia mgomo aliofanya kudai stahiki zake
Kukosekana kwake ni sababu nyingine inayoongeza hofu kwa Yanga ambayo itamtegemea zaidi kinda Ramadhani Kabwili
Kwenye mchezo wa kesho Simba inatarajiwa kuendeleza pale ilipoishia katika mchezo dhidi ya Al Ahly.
Ni mchezo ambao Simba inahitaji kushinda ili kuongeza 'mzuka' wa kula viporo ili kuhakikisha ubingwa wa ligi kuu unabakia Msimbazi