Baada ya kikosi chake kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui Fc katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara uliopigwa jana kwenye dimba la Taifa, kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi siku ya Jumanne, Februari 12 Simba itakapokuwa inachuana na Al Ahly katika mchezo wa ligi ya mabingwa barani Afrika
Akizungumzia mchezo wa jana, Aussems alisema wachezaji wake walicheza vizuri kwenye kipindi cha kwanza na kufanikiwa kufunga mabao matatu yaliyowahakikishia alama tatu muhimu
Amesema walihitaji matokeo ya ushindi katika mchezo huo na sasa wanaelekeza nguvu zao kwenye mchezo ujao dhidi ya Al Ahly
"Nawaomba mashabiki wote wa soka nchini bila ya kujali timu zao wajitokeze uwanja wa Taifa Jumanne. Naamini tukiwa na mashabiki zaidi ya elfu 50 uwanjani, hali ya hewa pamoja na ubora wa kikosi chetu unatupa matumaini ya kushinda mchezo huo," amesema Aussems
"Hata kama tulifungwa mabao 5-0 katika mchezo uliopita, nawaambie mchezo ujao utakuwa tofauti kabisa"
Simba itachuana na Al Ahly katika mchezo ambao inahitaji kushinda ili kuweka hai matumaini ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya vilabu