Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara Simba wamerejea kwa kishindo katika ligi hiyo mwaka 2019 kwa kuifumua Mwadui Fc mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa dimba la Taifa Alhamisi jioni
Simba ilifunga mabao yake yote kwenye kipindi cha kwanza kupitia kwa Meddie Kagere aliyefunga bao la kwanza kwenye dakika ya 21, Mzamiru Yassini (26') na John Bocco aliyefunga bao la tatu kwenye dakika ya 29
Simba iliuanza mchezo huo kwa kasi na ilifanikiwa kutawala kwa muda mwingi hasa kwenye kipindi cha kwanza huku Mwadui Fc ikitumia mashambulizi ya kushitukiza
Kocha Patrick Aussems alifanya mabadiliko kidogo ya kikosi chake kilichoanza ambapo aliwaanzisha Haruna Niyonzima, Mzamiru Yassini, Paul Bukaba na Zana Coulibaly huku Jonas Mkude, Rashidi Juma na Emmanuel Okwi wakianzia benchi


Simba ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini washambuliaji wake bado wanashindwa kuzitumia ipasavyo
Leo Simba ingeweza kufunga zaidi ya mabao matano kama Bocco, Okwi na Niyonzima wangeweza kutumia nafasi walizopata kwenye mchezo huo
Ushindi huo umeirejesha Simba kwenye nafasi ya tatu baada ya kufikisha alama 36 na kuzipiku Lipuli Fc na KMC
Matokeo hayo pia yana maana kubwa kwa wachezaji wa Simba kwani yameongeza morali yao kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Al Ahly utakaopigwa Jumanne ijayo katika dimba la Taifa