Keshokutwa kikosi cha Simba kitacheza mchezo wa mzunguuko wa 25 wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mwadui Fc
Mchezo huo utapigwa Alhamisi, Februari 07 katika dimba la Taifa saa moja usiku
Wakati ligi ikiwa imebaki takribani miezi mitatu iweze kumalizika, Simba italazimika kucheza michezo 24 katika kipindi hicho kutokana na kuwa na idadi ya mechi nyingi za viporo
Michezo ya Simba itakuwa ikitofautiana kwa siku tatu hadi nne ili kuweza kuzifikia timu nyingine ambazo tayari baadhi zimecheza mechi 10 zaidi
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema walitarajia kukumbana na ratiba ya aina hii kutokana na muda uliobaki kabla ya ligi kumalizika
Lakini Mbelgiji huyo amesema watahakikisha wanapambana waweze kutetea ubingwa wao ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya Kimataifa msimu ujao.
Baada ya kutolewa kwenye michuano ya kombe la FA, Simba ni lazima itwae ubingwa ili iweze kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa mwakani
Baada ya mchezo wa Feb 07, Simba itachuana na Al Ahly Feb 12 katika mchezo utakaopigwa dimba la Taifa.
Februari 16 itachuana na Yanga na Feb 19 itaelekea mkoani Arusha kuikabili African Lyon.
Feb 22 itarejea jijini Dar es salaam kuikabili Azam Fc na Feb 26 itakwenda Iringa kuikabili Lipuli Fc
Mwanzoni mwa mwezi wa tatu itasafiri kuelekea nchini Algeria kuikabili JS Saoura kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa kabla ya kurejea jijini Dar es salaam kumalizana na Vita Club wiki moja baadae
Kimahesabu mpaka sasa Simba inaweza kufikisha alama 54 na kuwa sawa na Yanga kama itashinda michezo yake saba ya viporo ili kufikisha idadi sawa ya michezo na Yanga
Kocha Aussems hapaswi kudharau mchezo wowote kwani Simba inahitaji kushinda michezo yake yote ya viporo ili kuweza kuzifikia Yanga na Azam Fc kwanza ambazo tayari zimeshuka dimbani mara 21 na 20