Kikosi cha wachezaji 20 na benchi la ufundi wanaondoka leo jioni kuelekea nchini Misri kwa ajili ya mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya vinara wa kundi D Al Ahly
Mchezo huo utapigwa February 02 katika jiji la Cairo saa nne usiku kwa saa za Tanzania
Simba imekwenda Misri ikiwa na matumaini ya angalau kuondoka na alama moja katika mchezo huo ambao utakuwa mgumu kutokana na mwenendo wa timu za Misri hasa zinapocheza nyumbani
Simba inatarajiwa kukutana na mazingira magumu ndani na nje ya uwanja.
Tayari baadhi ya viongozi wa Simba walishatangulia nchini Misri kuandaa mazingira mazuri kwa kikosi cha Simba kitakapowasili nchini humo
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wanakwenda Misri wakitambua ugumu wa timu watakayokutana nayo
Amesema watapambana mpaka dakika ya mwisho kuhakikisha wanapata matokeo mazuri
Zahera atoa ushauri
Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera mara kadhaa amekuwa akitoa maoni na ushauri kwa Simba kufanya vizuri katika michuano hiyo.
Amesema wachezaji wanapaswa waandaliwe kiufundi kwa asilimia 40 na asilimia nyingine 60 zitumike kuwaandaa kisaikolojia kabla ya kuwakabili Al Ahly
Zahera amesema wachezaji wa Simba wanapaswa wasahaulishwe matokeo ya mchezo uliopita, waingie katika mchezo huo wakiwa na fikra mpya
"Wachezaji bado wana maumivu ya matokeo waliyopata katika mchezo uliopita, inapaswa wasaidiwe kusahau," amesema
Amesema Simba inaweza kufungwa idadi kubwa ya mabao kama wachezaji wataingia kwenye mchezo huo wakiwa bado na mawazo ya kipigo cha Vita Club