Imeelezwa siku moja kabla ya mchezo dhidi ya Bandari Fc wachezaji saba wa kikosi cha Simba walitoroka kambini usiku na kwenda 'kujiachia'
Kulingana na taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, juzi usiku viongozi wa Simba walivamia ghafla kambi ya Simba na kubaini wachezaji saba hawakuwepo
Wachezaji wanaotajwa kukosekana usiku huo ni Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Shiza Ramadhani Kichuya, Jonas Mkude, Pascal Wawa na Mohamed Ibrahim 'MO'
Miongoni mwa wachezaji hao, Hassani Dilunga na Mzamiru Yassini walianza katika mchezo dhidi ya Bandari Fc, Mzamiru akihusika kwenye bao la kwanza la Bandari Fc baada ya kusababisha penati huku mwenyewe akiumia na kulazimu akimbizwe Hospitalini
Aidha inaelezwa viongozi wa benchi la Ufundi wakiongozwa na kocha Patrick Aussems walishangazwa na taarifa za kutoonekana kwa wachezaji hao wakiwa hawafahamu walipokuwa wamekwenda
Uongozi wa Simba haujatoa taarifa rasmi juu ya ukweli wa tuhuma hizi zinazowakabili baadhi ya wachezaji wake waandamizi
Lakini ni dhahiri tukio hilo halitoi picha nzuri kuhusu nidhamu ya baadhi ya wachezaji wa Simba