Kikosi cha Simba leo kimeendelea na mazoezi kwenye dimba la Boko Veterans kujiandaa na mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Al Ahly utakaopigwa Februari 02 huko nchini Misri
Lakini kabla ya safari ya Misri, kesho Simba itashuka katika dimba la Taifa kuikabili Mbao Fc kwenye mchezo wa kusaka mshindi wa tatu michuano ya SportPesa Cup
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amewataka mashabiki wa timu hiyo wasahau matokeo ya michuano ya SportPesa na waendelee kuiunga mkono timu yao inayokabiliwa na michezo muhimu ya ligi ya mabingwa
Simba inayoshika nafasi ya tatu kundi D michuano ya ligi ya mabingwa, bado ina nafasi ya kutinga robo fainali kama itaweza kupata angalau alama moja katika michezo miwili ya ugenini iliyobaki na ikafanikiwa kushinda michezo yake yote miwili ya nyumbani
Bocco arejea kikosini
Nahodha wa kikosi cha Simba John Bocco amepona majeraha na amerejea rasmi kikosini
Bocco aliumia katika mchezo wa kwanza wa ligi ya mabingwa dhidi ya JS Saoura
Wakati Bocco akianza mazoezi kamili, kiraka Erasto Nyoni ameanza mazoezi mepesi atakuwa tayari kurejea kikosini wiki ijayo