Hakuna ubishi ukizungumzia timu pendwa zaidi hapa Tanzania ni Simba. Ukitaka ujue ukubwa wa Simba angalia jinsi mashabiki wa timu hiyo wanavyojitoa hasa inapocheza 'michezo mikubwa' kwenye dimba la Taifa
Simba imekuwa na kawaida ya kujaza uwanja wa Taifa unaochukua mashabiki takribani elfu 60.
Kwa miaka ya hivi karibuni barani Afrika hakuna timu iliyokuwa na ubavu wa kufanya hivyo zaidi ya Simba
Hata hivyo mwenendo wa timu umeanza kuwakatisha tamaa wadau ambao wanaona wachezaji wa timu hiyo pengine hawafahamu ukubwa wa timu wanayocheza
Jana Simba imeondoshwa kwenye michuano ya SportPesa Cup na Bandari Fc kwa kufungwa mabao 2-1.
Ni matokeo ambayo hayakutarajiwa na hakika yamewaumiza Wana Msimbazi kwani hakuna aliyekuwa amejiandaa na matokeo hayo
Sawa, mpira una matokeo matatu, lakini wengi walitarajia Simba ingetwaa taji la SportPesa hasa ikizingatiwa ndio timu bora zaidi kwa ukanda wa Afrika Mashariki kwa sasa
Simba ndio klabu pekee ambayo imetinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa kutoka Afrika ya Mashariki
Pia ndio timu yenye wachezaji bora, mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji 'MO' ametimiza wajibu wake.
MO ametoa na anaendelea kutoa fedha za usajili, anawalipa wachezaji mishahara mizuri. Kiufupi hakuna timu yenye mazingira mazuri ya kiuchumi kama ilivyo Simba kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki
Hata hivyo licha hayo yote, wachezaji wa Simba wamemwangusha mwekezaji wao, mashabiki wao na wadau wanaojitoa kuhakikisha wanapata kila wanachotaka
Simba hii pia iliondoshwa kwenye michuano ya kombe la FA na timu ya daraja la kwanza, Mashujaa Fc kutoka mkoani Kigoma.
Ikashiriki michuano ya kombe la Mapinduzi, ikafungwa na Azam Fc kwenye mchezo wa fainali
Wengi walitarajia michuano hii ya kombe la SportPesa wangeitumia ipasavyo kwa kushinda taji ili kuwapa imani mashabiki wao
Simba imesalia na michuano miwili ligi ya mabingwa na ligi kuu ambayo pia ina ugumu wa aina tofauti
Wakati ikiwa tayari imefikia malengo ya mwaka huu ya kutinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa, kwenye ligi bado watalazimika kufanya kazi ya ziada ili kutetea ubingwa
Simba ina idadi kubwa ya michezo ya viporo (nane) lakini kama wachezaji hawatajitoa huenda kazi ya kutetea ubingwa ikawa ngumu kuliko inavyofikiriwa
Ni kawaida kwa ligi kuwa ngumu hasa katika raundi ya pili kutokana na baadhi ya timu kupigania zisiteremke daraja
Bahati mbaya Simba itakutana na baadhi ya timu hizo katika michezo ya viporo.
Hivi wachezaji wa Simba mtaficha wapi sura zenu kama Simba itashindwa kutwaa taji lolote msimu huu?
Na hatari inayokuja mbeleni ni kukosa kushiriki michuano ya Kimataifa msimu ujao kama Simba itashindwa kutetea ubingwa au kutwaa taji la ligi ya mabingwa