Vinara wa kundi D michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, Simba keshokutwa Jumamosi watakuwa dimbani nchini Congo kupepetana na Vita Club katika mchezo unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali
Mchezo huo utapigwa saa moja usiku kwa saa za Tanzania katika dimba la Stade des Martyrs linalochukua mashabiki takribani 80,000/-
Vita inatajwa kuwa miongoni mwa timu ngumu kufungika inapocheza katika dimba lake la nyumbani.
Tangu mwaka 1971 timu hiyo imefungwa mara tatu tu katika michezo ya vilabu barani Afrika iliyocheza nyumbani.
Aidha kipigo cha mabao 2-0 walichopata kutoka kwa Al Ahly katika mchezo wa kwanza nchini Misri kimeufanya mchezo huo kuwa ni lazima kushinda kwa Wacongomani hao
Hata hivyo yatakuwa makosa makubwa kwa mtu yeyote kudhani AS Vita itapata mteremko kwa Simba.
Simba inayonolewa na kocha Patrick Aussems imejipambanua kuwa timu inayoweza kupata matokeo bila ya kujali inacheza nyumbani au ugenini.
Mfano mzuri ni mchezo dhidi ya Mbabane Swallows ambao Simba ilishinda mabao 4-1 kwenye uwanja wa Taifa na ugenini wakashinda kwa mabao 4-0
Simba ya sasa iko imara kutokana na kuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu wa kucheza michezo ya Kimataifa
Aishi Manula, Paschal Wawa, Juuko Murshid, Clatous Chama, Meddie Kagere, James Kotei, Jonas Mkude na Emmanuel Okwi ni miongoni mwa wachezaji wa Simba ambao 'wamekomaa' na wanaweza kuleta upinzani kwa timu yoyote barani Afrika.
Simba itashuka dimbani ikiwa haina presha ya matokeo tofauti na wapinzani wao ambao tayari wamepoteza mchezo wao wa kwanza.
Ushindi au sare kwa Simba ni matokeo mazuri wakati Wacongomani hao watalazimika kusaka ushindi hali inayoweza kuipa nafasi Simba kupata matokeo
Kabla ya kikosi chake kukwea pipa leo kwenda Congo, Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema wanakwenda Congo kupambana.
Amesema katika mchezo huo Simba haitacheza kwa kujihami kama zifanyazo timu nyingi zinapokua ugenini.