Kiungo fundi Haruna Niyonzima jana aliisaidia Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mlandege Fc kwenye mchezo wa kombe la Mapinduzi kundi A.
Niyonzima alifunga bao pekee la Simba kupitia mkwaju wa penati na kuwahakikishia mabingwa hao wa Tanzania Bara ushindi wa tatu mfululizo na kumaliza hatua ya makundi wakiwa wameshinda michezo yote.
Simba imetinga nusu fainali ya michuano hiyo ikiwa kileleni mwa kundi A baada ya kujikusanyia alama tisa.
Niyonzima alikuwa katika kiwango bora kwenye mchezo huo na haikushangaza kwa yeye kuteuliwa kuwa nyota wa mchezo na kukabidhiwa zawadi ya mpira na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mohamed Ahmada
Bila shaka kocha Patrick Aussems amemuona na huenda akampa nafasi kwenye mchezo ujao wa ligi ya mabingwa dhidi ya JS Sauora,kutegemeana na mahitaji ya timu.
Niyonzima anakabiliwa na ushindani mkali wa namba kutoka kwa viungo wanaon'gara zaidi kwa wakati huu katika kikosi cha Simba Clatous Chama 'CCC' na Hassan Dilunga 'HD'