Kinara wa mabao wa kikosi cha Simba Meddie Kagere, amesema licha ya ushiriki wao kwenye Kombe la Mapinduzi linaloendelea visiwani Zanzibar, mawazo yao yapo kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya JS Saoura ya Algeria.
Simba itakuwa mwenyeji wa timu hiyo anayochezea Mtanzania Thomas Ulimwengu Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kagere, alisema mchezo huo wa kwanza ni muhimu sana kujiweka katika mazingira mazuri ya ushindani kwenye kundi lao hilo la D lenye timu nyingine za Al Ahly ya Misri na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Alisema michezo wanayocheza Zanzibar kwenye michuano hiyo ya Mapinduzi ni sehemu ya maandalizi yao kuelekea kwenye mchezo huo muhimu.
“Kila mchezaji anataka kuona tunafanya vizuri kwenye mchezo huo, mimi pia naamini tuna nafasi ya kushinda, kwetu michezo ya Mapinduzi ni sehemu ya maandalizi japo pia tunataka kufanya vizuri kwenye michuano hii ya Mapinduzi,” Kagere amenukuliwa na gazeti la Nipashe.
Alisema msimu huu wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye michuano hiyo ya CAF, lakini pia kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Tumejipanga na tunaendelea kujipanga kuhakikisha tunafanya vizuri katika kila mashindano tunayoshiriki, tunataka kuona tunafika mbali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, pia kutetea ubingwa wa Ligi Kuu,” alisema kagere.
Aidha, alisema yote hayo yanawezekana kama watapambana ndani ya uwanja katika michezo yao yote.
Kagere ameifungia Simba mabao mawili kwenye mchezo wa kwanza wa kombe la Mapinduzi dhidi ya Chipukizi ambao Simba waliibuka na ushindi wa mabao 4-1.
Katika mchezo wa jana dhidi ya KMKM Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 huku Kagere akipumzishwa.