Simba yapewa 'mchongo' wa kuimaliza JS Saoura

Mwana Msimbazi By Mwana Msimbazi
β€’
5 Jan 2019
Simba yapewa 'mchongo' wa kuimaliza JS Saoura

Wawakilishi wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba wana kila sababu ya kuibuka na ushindi kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saouram Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa.

Rekodi ya kibabe ambayo Simba imekuwa nayo kwenye mashindano ya kimataifa pindi inapocheza nyumbani inaweza kuwa na mwendelezo mzuri mbele ya Saoura ambayo yenyewe imekuwa haifanyi vizuri ugenini.

Katika mechi tatu za mwisho za kimataifa ambazo Simba imecheza nyumbani, imepata ushindi mara mbili na kutoka sare moja huku ikifunga jumla ya mabao 10 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne.

Wakati Simba ikijivunia rekodi hiyo, Saoura yenyewe imekuwa haina rekodi nzuri ugenini kwani katika michezo mitatu ya kimataifa iliyocheza kwenye viwanja vya ugenini msimu huu na ule wa 2007, imetoka sare mara mbili kufungwa moja huku ikiwa haijapachika hata bao moja na yenyewe imeruhusu nyavu zake zitikiswe mara moja.

THAMANI YA VIKOSI

Sahau kidogo kuhusu matokeo ya mchezo huo ambayo kila timu inapigia hesabu ya pointi tatu, jambo lingine linaloweza kuipa mzuka Simba ni hamu ya kuwazima nyota wenye thamani kubwa wa JS Saoura ambayo thamani ya kikosi chake kwa ujumla ni kiasi cha Euro 7.2 milioni (zaidi ya Shilingi 18 bilioni za Tanzania).

Kikosi cha kwanza tu cha Saoura kinachoundwa na kundi kubwa la nyota kutoka Algeria na wachache wanaotoka nje ya nchi hiyo, kina thamani ya Sh 9.1 bilioni, fedha ambayo ni mara nane ya thamani ya kikosi cha Simba ya Shilingi 1.3 bilioni.

Wakati mchezaji mweye thamani kubwa zaidi kwenye kikosi cha Simba akiwa ni Cletous Chama ambaye Mtandao wa Transfermarkt umemtaja kuwa na thamani ya Euro 100,000, upande wa Saoura mchezaji mwenye thamani kubwa ni kiungo mshambuliaji Messalla Merbah mwenye thamani ya Euro 500,000 (zaidi ya Sh 1.3 bilioni).

Mchezaji mwenye thamani ya chini zaidi katika kikosi cha Simba ni Erasto Nyoni ambaye dau lake ni Sh 35 milioni wakati kwa upande wa Saoura ni beki Nacereddine Khoualed ambaye thamani yake ni Euro 200,000 (zaidi ya Sh 524 milioni).

MBINU UWANJANI

Simba inapaswa kuwa makini mno na mbinu ya kupiga mashuti ya mbali ambayo Saoura imekuwa ikitumia kwenye mechi mbalimbali inazocheza hasa zile ambazo huwa inazidiwa.

Saoura imekuwa ikimtumia zaidi kiungo wake mshambuliaji Messalla Merbah mwenye umri wa miaka 27 ambaye amekuwa na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti ya nje ya eneo la hatari pindi anapopasiwa na wenzake au anapoukuta mpira uliookolewa na timu pinzani.

Saoura pia ni wajanja katika kufunga mabao kupitia mipira ya kona na adhabu ndogo kuelekea lango la timu pinzani.

Safu ya ulinzi ya Simba inapaswa kucheza kwa umakini na tahadhari kubwa zaidi pindi inapowazuia nyota wa Saoura hasa mshambuliaji Mohamed Hammia kutokana na ujanja wa wapinzani wao hao katika kujiangusha ndani ya boksi la timu pinzani ili wapatiwe penati.

Na kwa kulidhihirisha hilo, katika mabao manne ambayo Saoura imeyafunga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, matatu yametokana na penalti za kujiangusha.

Kwa upande wa Simba yenyewe imekuwa ikibebwa na mbinu ya kushambulia kwa kushitukiza ikiingia kwa haraka eneo la timu pinzani baada ya kupora mpira lakini wakati mwingine hutumia mbinu ya kupiga pasi nyingi fupifupi kwa ajili ya kujenga mashambulizi.

MIFUMO

Hapana shaka Simba itatumia mfumo wake wa 4-3-3 kwa kuendelea kuwapanga Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco upande wa ushambuliaji, huku nyuma yao wakiwepo Chama, Jonas Mkude na James Kotei kwenye kiungo.

Mfumo huu wa Simba umekuwa ukibadilika hasa pale inapowaingiza Shiza Kichuya na Hassan Dilunga ambapo hucheza mfumo wa 4-4-2 wa dhahabu

Upande wa Saoura yenyewe imekuwa ikipendelea kutumia mfumo wa 4-4-2 asilia wa kuwa na mawinga wawili na viungo wawili.

Hata hivyo, mawinga wa Saoura, Younes Koulkheir na Hamza Zaidi ni wa kuchungwa mno kwani wamekuwa na uwezo wa kuingia ndani na kucheza kama viungo pindi wanapokutana na timu iliyo imara sehemu ya katikati.

NYOTA WA KUCHUNGWA

Wakati Cletous Chama akitajwa kuwa ndiye mtu ambaye Waarabu watapaswa kumchunga zaidi, Simba inatakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha, inawaficha mshambuliaji Mohamed Hammia na kiungo mshambuliaji Messalla Merbah ambao ndio wamekuwa uti wa mgongo wa Saoura.

Merbah amekuwa na uwezo mkubwa wa kufunga mabao kwa mashuti ya mbali wakati Hammine ni msumbufu kwa mabeki, ana utulivu na uwezo wa hali ya juu kufumania nyavu lakini pia ni mchezaji anayeweza kumdanganya mwamuzi na kuomba penalti.

VIKOSI

Katika hali ya kushangaza, wastani wa umri kwa vikosi vya timu zote mbili ni miaka 27.71 ambapo mchezaji mdogo zaidi akiwa ni Mohammed Hussein 'Tshabalala' aiyezaliwa Novemba Mosi,1996 wakati mchezaji mkubwa zaidi ni kipa wa Saoura, Abderraouf Nateche mwenye umri wa miaka 36.

kikosi cha Simba na umri wake kwenye mabano ni Aishi Manula (22), Nicholas Gyan (29), Mohammed Hussein (22), Erasto Nyoni (30), Paschal Wawa (32), James Kotei (25), Cletous Chama (27), Jonas Mkude (26), Meddie Kagere (32), John Bocco (29) na Emmanuel Okwi (260

Kikosi cha Saoura Abderraouf Nateche (36), Fateh Talah (25),Elhadji Konate (24), Ibrahim Elkhalil Bekakchi (26), Nacereddine Khoualed (32), Adel Bouchiba (30), Hamza Zaidi (28), Messalla Merbah (27), Mohammed Hammia (27), Mohamed Boulaouidet (28) na Younes Koulkheir (22)

NANI KUMDHIBITI NANI

Wakati mwingine fedha inaweza isiwe sababu ya timu kupata matokeo. Nje ya uwanja, wachezaji wa Saoura wana thamani kubwa kuliko wale wa Simba lakini hilo halifanyi waweze kupata ushindi kirahisi Jumamosi ijayo.

Simba ina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi ikiwa nyota wake watajiandaa vizuri kimbinu na kiufundi na kucheza vizuri zaidi kuliko Saoura hiyo Jumamosi.

Nyota wa Simba watakuwa na kazi ya kuonyesha kuwa thamani ya wachezaji wa Saoura sio kitu kwa jinsi kila mmoja atakavyoweza kumdhibiti mtu atakayekabiliana naye.

Mwanaspoti

ADVERTISE HERE

Simba SC Stories

Mkutano Mkuu Simba sasa ni Januari 2027
Mkutano Mkuu Simba sasa ni Januari 2027
1h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
5h ago
READ MORE β†’
Mechi dhidi ya Fountain Gate yasogezwa mbele kwa siku moja
Mechi dhidi ya Fountain Gate yasogezwa mbele kwa siku moja
17h ago
READ MORE β†’
Simba kumuongeza Barker mkataba wa muda mrefu
Simba kumuongeza Barker mkataba wa muda mrefu
23h ago
READ MORE β†’
Simba yaifuata Fountain Gate Manyara
Simba yaifuata Fountain Gate Manyara
1d ago
READ MORE β†’
Hii hapa miamba 16 makundi CAFCL
Hii hapa miamba 16 makundi CAFCL
1d ago
READ MORE β†’
Highlights; Simba 3-0 15 de Agosto, CAFCL (FT)
Highlights; Simba 3-0 15 de Agosto, CAFCL (FT)
1d ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumatatu, Oktoba 26 2026
Magazeti ya leo Jumatatu, Oktoba 26 2026
1d ago
READ MORE β†’
FT : Simba 3-0 15 de Agosto, makundi CAFCL kibabe
FT : Simba 3-0 15 de Agosto, makundi CAFCL kibabe
1d ago
READ MORE β†’
Goals : Simba 3-0 15 de Agosto, CAFCL (FT)
Goals : Simba 3-0 15 de Agosto, CAFCL (FT)
1d ago
READ MORE β†’