Simba imedhamiria hasa kufafanya vizuri kwenye hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika ikitarajiwa kushuka dimbani Jumamosi Januari 12, 2019 kuikabili JS Sauora kwenye mchezo wa kwanza wa kundi B.
Moja ya mambo ambayo yamefanywa na uongozi wa timu hiyo ni kuhakikisha benchi la ufundi linapatiwa taarifa sahihi kuhusu wapinzani wao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Swedy Mkwabi amesema mara baada ya kupangwa kwa hatua ya makundi na kuwafahamu wapinzani wao, walifanya jitihada za kupata mikanda ya video ya timu zote walizopangwa nazo
"Tumetafuta kila kitu kinachohusiana na wapinzani wetu kama mikanda na video za mechi zao tayari zipo mikononi mwetu. Lengo ni kocha pamoja na wachezaji waanze kufanyia kazi mara moja kutokana na aina ya mashindano yenyewe yanahitaji umakini mkubwa," Mkwabi amenukuliwa na gazeti la Championi
"Na hiyo mikanda ambayo tumeipata na kumpatia mwalimu ni timu zote ambazo tumepangwa nazo katika Kundi D na tulitafuta mapema kumrahisishia kazi kocha wetu kuelekea mashindano hayo"
"Lakini kama timu malengo yetu ni kufanya vyema katika Ligi ya Mabingwa, kwa sasa tuna majukumu ya mapinduzi lakini maandalizi yanaendelea."
Simba imedhamiria kutinga robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kabisa barani Afrika kwa ngazi ya vilabu.
Ili kulifanikisha hilo Simba inapaswa kumaliza kwenye moja na nafasi mbili za juu kundi D linaloundwa na timu za Al Ahly, AS Vita, Simba na JS Sauora
Januari 12 itaanzia kampeni yake nyumbani kwa kuchuana na Sauora kabla ya kuelekea nchini Congo kuikabili Vita Club, Januari 19 2019