Baada ya droo ya hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa kufanyika nchini Misri wiki iliyopita na Simba kupangwa kundi D pamoja na mabingwa kihistoria wa michuano hiyo Al Ahly, AS Vita Club na JS Souara kutoka nchini Algeria , baadhi ya wachambuzi wa soka nchini wameipa Simba nafasi ndogo ya kufanya vizuri.
Wengi wanaotoa maoni hayo wanamezwa na majina ya timu bila ya kufahamu kuwa soka la Afrika sasa limebadilika sana ukilinganisha na miaka 10 iliyopita.
Juzi Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems aliwahakikishia Wana Msimbazi kuwa kila timu ina nafasi sawa ya kufuzu kutoka kundi D.
Aussems alisema timu zote zilizopangwa kundi D zinacheza mpira mzuri na kubainisha ushindani utakuwa mkubwa sana lakini maandalizi mazuri yataisaidia Simba kufanya vizuri.
Simba tayari imeanzisha mkakati wa kuhakikisha inatinga robo fainali ya michuano hiyo kipaumbele cha kwanza ikiwa ni kushinda michezo yake yote ya nyumbani.
Kama Simba itafanikiwa kupata alama zote tisa za nyumbani, ugenini hata ikipata alama mbili au tatu, kwa uzoefu wa michuano hiyo, alama 11 au 12 zinaweza kuivusha Simba kutinga robo fainali.
Wana Msimbazi wameaswa kuwa wamoja wakati huu kuipa sapoti timu yao kwenye michuano hiyo ili kuhakikisha inatinga robo fainali.
Simba ina historia ya kipekee katika michuano ya Afrika. Mwaka 2003 Simba iliwatoa mabingwa watetezi Zamalek na kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa.
Hivyo hii sio mara ya kwanza kwa Simba kupangwa na timu za Waarabu na mabingwa hao wa Tanzania Bara wana rekodi ya kipekee wanapokutana na timu za kiarabu.
Kwa wale wanaodhani Simba ndio mnyonge wa kundi D ni vyema wakaweka akiba ya maneno.