Mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Simba dhidi ya Singida United utapigwa keshokutwa Jumamosi, Disemba 29 saa moja usiku kwenye uwanja wa Taifa.
Mchezo huo ambao awali ulikuwa umepangwa kupigwa siku ya Jumapili, ulirudishwa nyuma kwa siku moja kutokana na uwanja wa Taifa kuwa na matumizi mengine siku hiyo.
Simba, Azam Fc na Yanga zote zinatarajiwa kushuka dimbani Jumamosi kucheza michezo yao ya kufunga mwaka 2018 kabla hazijaelekea visiwani Zanzibar kushiriki michuano ya kombe la Mapinduzi.

Msimu uliopita Simba ina kumbukumbu ya kushinda mabao 4-0 dhidi ya Singida United katika mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa na baadae kushinda kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa raundi ya pili uliopigwa mkoani Singida.
Simba inahitaji kushinda mchezo huo ili kuendelea kuzikimbiza Yanga na Azam Fc zilizo nafasi za juu kwenye msimamo lakini pia zikiwa zimecheza michezo mingi zaidi ya mabingwa hao watetezi.
Yanga inayoongoza ligi ikiwa na alama 47 imeshuka dimbani mara 17, Azam Fc inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 40 baada ya kushuka dimbani mara 16 wakati Simba imeshuka dimbani mara 13 tu ikiwa na alama 30.