Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema sababu iliyopelekea timu yake kupoteza mchezo wa kombe la FA jana dhidi ya Mashujaa ni kiwango cha chini kilichoonyeshwa na wachezaji wake hasa chipukizi.
Aussems amesema hakufurahishwa na matokeo hayo lakini yamechangiwa na makosa yaliyofanywa na wachezaji wenyewe.
"Baadhi ya wachezaji wetu walicheza chini ya kiwango," alisema Aussems baada ya mchezo huo uliomalizika kwa Simba kufungwa mabao 3-2
"Morali ya baadhi ya wachezaji ilikuwa chini sana na hata wakati wa mapumziko niliwatahadharisha kuwa ni lazima wajitoe ili timu iweze kupata ushindi na wasidhani kwa kuwa wanacheza na timu ya daraja la chini matokeo yatakuja tu"
"Lakini katika kipindi cha pili wachezaji walirudi na mitazamo ileile na matokeo yake tumepoteza mchezo muhimu. Nimehuzunishwa sana na matokeo haya na viwango vya baadhi ya wachezaji hasa chipukizi vimenisikitisha zaidi"
Kwa msimu wa pili mfululizo Simba inaondoshwa kwenye raundi ya tatu ya michuano ya kombe la FA (ASFC). Lakini msimu huu maumivu yamekuwa zaidi kwa kuwa uongozi wa timu hiyo ni kama haukujifunza na kilichotokea msimu uliopita, wakarudia makosa yaleyale.
Katika hatua nyingine Msemaji wa Simba Haji Manara amewataka mashabiki na Wanachama wa timu hiyo wasahau matokeo hayo na kujipanga kwa ajili ya michuano iliyo mbele yao.
"Matokeo haya tumeyasabisha sisi wenyewe, hatukupaswa kuidharau timu ya Mashujaa Fc," amesema Manara.
"Lakini tayari yameshatokea, tumetolewa kwenye mashindano sasa ni vyema tukaendelea kuwa wamoja tuangalie michuano inayotukabili mbele yetu"