Afisa Habari wa Simba Haji Manara ameeleza kusikitishwa na matokeo ya leo ya mchezo wa kombe la FA ambapo Simba imelazwa mabao 3-2 na Mashujaa Fc na kuondoshwa kwenye michuano ya kombe la FA (ASFC)
Bila ya kumumunya maneno, Manara amesema dharau iliyoonyeshwa na Simba kwa Mashujaa FC ndio iliyowagharimu mabingwa hao wa Tanzania Bara.
"Hakuna kitu kibaya kama dharau na tunawaumiza washabiki wetu! Simba ni klabu kubwa sana na hilo kila mtu klabuni alijue!! Okey maisha lazima yasonge mbele," ameandika Manara katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram
Wengi wameshangazwa na uamuzi wa kocha Patrick Aussems kufanya mabadiliko makubwa ya kikosi wakati inafahamika michuano ya kombe la FA ni ya mtoano.
Athari ya matokeo haya ni kubwa kwani yanaweza kuinyima Simba nafasi ya kushiriki michuano ya Kimataifa msimu ujao kama itashindwa kutetea ubingwa wake au kutwaa taji la Ligi ya mabingwa Barani Afrika.