Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema ushindi wa jana dhidi ya Nkana Fc ni zawadi kwa Mwekezaji wa klabu hiyo Mohammed Dewji 'MO' na mashabiki wa timu hiyo.
Aussems ameingia kwenye historia ya mabingwa hao wa Tanzania Bara baada ya kufanikiwa kuwapeleka hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3 dhidi ya Nkana FC.
Mara ya mwisho Simba ilifuzu hatua hiyo mwaka 2003 na hakuna timu nyingine ya Tanzania iliyofanikiwa tangu wakati huo kabla ya Simba kufuzu kwa mara nyingine hapo jana.
"Mafanikio haya ni zawadi kwa Mwekezaji wetu MO Dewji na mashabiki wote wa Simba"
"Wachezaji wetu walicheza vizuri na wamestahili ushindi huu. Nawapenda wote, tusherehekee XMas kwa furaha," umesomeka ujumbe wa Aussems.
Droo ya hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa itafanyika Ijumaa ya wiki hii Simba ikiwa miongoni mwa timu 16 zinazosubiri kushiriki hatua hiyo.