Bao la 'kideo' lililowekwa kambani na Mzambia Cleotus Chama kwenye dakika ya 88 limeipeleka Simba hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
Chama amehusika katika mabao mawili yaliyofungwa na Simba leo kwenye ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Nkana Fc.
Alitengeneza bao la kwanza la Simba lililofungwa kwa shuti la Jonas Mkude kwenye dakika ya 29 na kuirudisha Simba mchezoni.
Lakini mjadala zaidi ni bao lake alilofunga kwa kisigino wakati mchezo huo ukielekea ukingoni.
Akiwa amezongwa na beki wa Nkana Fc Chama aliweza kuunganisha kwa kisigino krosi ya chini ya kiungo Hassani Dilunga kutoka upande wa kushoto.
Mabao aina ile yanafungwa na wachezaji wanaoujua mpira hakika Chama ameonyesha kuwa na uwezo mkubwa.
Mzambia huyo amewaziba midomo wale waliokuwa wanamkosoa aliposhindwa kun'gara kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Zambia na Simba kufungwa mabao 2-1.