Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amebainisha kuwa kikosi chake kipo tayari kwa asilimia 100 kuelekea mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) dhidi ya Orlando Pirates.
Mchezo huo unaotarajiwa kuwa wa vuta-nikuvute utapigwa kesho Jumapili saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea pambano hilo, Barker alikiri kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kwa timu zote mbili, lakini akasisitiza kuwa kikosi chake kimeshafikia asilimia 80 ya kiwango anachokihitaji ili kupata matokeo chanya.
"Ugumu wa mechi hii hauikabili Simba pekee, bali hata Orlando Pirates watakutana na mpinzani imara. Hatujapoteza mchezo wowote msimu huu, na tuko nyumbani," alisema Barker akijiamini.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini aliongeza kuwa anaijua vizuri sana Orlando Pirates, mifumo yao, na hata baadhi ya wachezaji na wafanyakazi wake wa zamani waliohamia klabuni hapo.
Hata hivyo, alikataa kuweka wazi mbinu zake za kiufundi akidai kuwa mikakati hiyo itabaki kuwa siri ya chumba cha kubadilishia nguo hadi dakika 90 zitakapoamua.
Licha ya changamoto ya majeraha inayowakabili walinzi Nathaniel Chilambo na Ismael Toure, Barker amewatoa hofu mashabiki wa Simba kwa kueleza kuwa kurejea kwa beki mzoefu Shomari Kapombe kunampa wigo mpana na utulivu katika safu yake ya ulinzi.
Barker amesisitiza umuhimu wa kuanza na ushindi nyumbani ili kuepuka makosa ya msimu uliopita ambapo timu ilianza kwa kusuasua na kulazimika kufukuzia alama mbeleni
Orlando Pirates wajawa hofu
Kwa upande wao, Kocha Mkuu wa Orlando Pirates, Abdeslam Ouaddou, amekiri wazi kuwa uzoefu mkubwa wa Barker katika soka la Afrika Kusini unawanyima usingizi.
Ouaddou alibainisha kuwa mchezo huo utakuwa mtihani mzito kabisa katika malengo yao ya kuusaka ubingwa wa Afrika msimu.