Kikosi cha Simba SC leo kinatarajiwa kuhitimisha maandalizi yake kuelekea mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Vijana wa kocha Steve Barker wamejichimbia kambini kwa takribani wiki moja sasa wakiandaa dozi maalumu kwa ajili ya The Buccaneers, kabla ya kushuka kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kesho Jumapili, Novemba 29.
Ni wazi hautakuwa mchezo mwepesi kwa pande zote mbili, lakini Wekundu wa Msimbazi wameweka wazi msimamo wao kuwa hakuna timu itakayotoka salama kwenye dimba la Uhuru katika hatua ya makundi msimu huu.
Pambano hilo pia linaweza kutafsiriwa kuwa mchezo wa kisasi kwa Mnyama dhidi ya Orlando Pirates, ambao mwaka 2022 waliizuia Simba kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Wakati huo, Pirates waliiondoa Simba kwa mikwaju ya penalti baada ya kila timu kushinda bao 1-0 katika uwanja wake wa nyumbani.
Safari hii, Simba inaingia kwenye pambano hilo ikiwa na morali kubwa kutokana na mwenendo wake mzuri katika mashindano yote tangu kuanza kwa msimu.
Mkufunzi wa Simba, Steve Barker, ameweka wazi dhamira yake ya kuendeleza mwanzo huo mzuri, huku akilenga kukiongoza kikosi chake kuvuna alama tatu muhimu dhidi ya wapinzani hao.
Mnyama ameweka rekodi ya aina yake katika Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kushinda michezo yote 11, huku pia akishinda michezo yote minne ya hatua za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika, akifunga mabao 16 na kuruhusu mabao mawili pekee.
Takwimu hizo zinaakisi uimara wa kikosi cha Barker katika maeneo ya ushambuliaji na ulinzi, silaha ambazo Simba inatarajia kuzitumia kuwanyamazisha wababe hao wa Afrika Kusini.
Huku kaulimbiu ya ‘HUYU NI WETU’ ikitawala miongoni mwa mashabiki wa Simba, Wekundu wa Msimbazi wamepania kuanza kwa kishindo safari yao ya kusaka tiketi ya hatua ya robo fainali.