Klabu ya Simba SC imezindua rasmi kampeni ya hamasa kuelekea mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, huku ikitangaza kaulimbiu ya ‘HUYU NI WETU’.
Uzinduzi huo umefanyika katika Tawi la Simba la Jangwani Mafuso, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhamasisha mashabiki kuelekea pambano hilo litakalopigwa Jumapili, Novemba 29, kwenye Uwanja wa Uhuru.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema mchezo huo ni muhimu katika safari ya Wekundu wa Msimbazi kuelekea kutimiza malengo yao ya kufika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Simba yataka alama tatu
Ahmed amesema licha ya ubora wa Orlando Pirates, Simba haina chaguo jingine zaidi ya kuhakikisha inapata ushindi katika mchezo huo, akisisitiza umuhimu wa kila Mwanasimba kujitoa kwa asilimia 100.
“Mechi ya Jumapili lazima tuambizane ukweli ni mechi ngumu kwelikweli. Ni mechi ambayo inatuhitaji Wanasimba kujitoa kwa asilimia 100 kuipambania Simba yake. Sio kazi ya Steve Barker peke yake, sio kazi ya Rushine peke yake ni kazi ya kila Mwanasimba.
“Na sisi tunasema iwe iwavyo, liwake inyeshe tarehe 29 hakuna kingine ambacho tunahitaji zaidi ya alama tatu dhidi ya Orlando Pirates,” amesema Ahmed.
Semaji huyo ameongeza kuwa Simba inalenga kutumia vyema faida ya kucheza nyumbani, huku akitamba kuwa Orlando Pirates haitakuwa na nafasi ya kutamba mbele ya Wekundu wa Msimbazi.
“Ushindi katika mchezo huu hautakuja kwa nyimbo pekee, utakuja kwa vitendo. Niwambie huyu Orlando anaweza kuwa mbabe kwao lakini sio katika tanuri la Mnyama, sio uwanja wa Uhuru. Atake asipende atapasuka.”
Tiketi 6,000 pekee zaruhusiwa
Akizungumzia suala la tiketi, Ahmed amesema tayari zimeanza kuuzwa kwa mfumo wa kidigitali, huku idadi ya mashabiki walioruhusiwa kushuhudia mchezo huo ikiwa ni 6,000 pekee.
Amewataka mashabiki kuhakikisha wanamaliza tiketi hizo mapema ili kuonyesha Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuwa idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa mchezo pamoja na wingi wa mashabiki wa Simba.
“Tunataka kuwaonyesha CAF kwamba idadi hii ya tiketi waliyotupa ni ndogo kwa kumaliza mapema tiketi hizo ili kuwapa nguvu viongozi wetu ya kuendelea kupambana ili tupate idadi kubwa ya mashabiki.”
Ahmed pia amesisitiza kuwa nguvu kutoka majukwaani itakuwa sehemu muhimu ya kuisaidia Simba kupata ushindi, akieleza matarajio yao ya kuifunga Orlando Pirates kwa angalau mabao mawili.
Dhamira ni Kufika Nusu Fainali
Mbali na kutaka kuanza vizuri hatua ya makundi, Simba imeweka wazi dhamira yake ya kurejea katika nafasi za juu za ubora wa klabu barani Afrika.
Kwa mujibu wa Ahmed, kushuka kwa Simba kutoka nafasi ya tano hadi ya 11 katika viwango vya ubora barani Afrika hakulingani na hadhi na malengo ya klabu hiyo.
“Safari hii sio kushiriki tu na kuishia makundi kama msimu uliopita, msimu huu tunaitaka kweli nusu fainali.”
Amesema ili kufanikisha malengo hayo, Simba inahitaji kuvuna alama zote tisa katika michezo yake mitatu ya nyumbani kwenye hatua ya makundi, kabla ya kutafuta alama nyingine ugenini.
Uchaguzi uwekwe pembeni
Ahmed pia ametumia uzinduzi huo kuwataka wanachama na mashabiki wa Simba kuweka kando tofauti zao zinazotokana na mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo na kuelekeza nguvu zao katika mchezo dhidi ya Orlando Pirates.
Amesisitiza kuwa licha ya kuwepo kwa makundi yenye mitazamo tofauti kuhusu uchaguzi, wakati huu ni muhimu kwa kila Mwanasimba kusimama pamoja kwa maslahi ya klabu.
“Mambo ya uchaguzi tunayaweka pembeni kwa siku chache, uchaguzi upo tu. Tukipoteza mechi ya Orlando tutakuwa na hali mbaya, uchaguzi ni mwakani, kilicho karibu ni mechi ya Orlando tuwekeze nguvu hapo.”
Aidha, amesisitiza umuhimu wa matawi katika kuimarisha uhai wa klabu hiyo, akiwataka Wanasimba kuendelea kuanzisha matawi katika maeneo wanayofanyia shughuli zao.
Simba inaelekeza nguvu zake zote katika pambano la Jumapili, huku ujumbe mkuu kwa mashabiki wake ukiwa ni umoja, kujitoa na kuipambania timu ili kupata alama tatu muhimu.
“Kitu kimoja pekee ndio kitatuvusha salama dhidi ya Orlando, kitu chenyewe ni Nguvu Moja,” amesema Ahmed Ally, akihitimisha kwa kutangaza kaulimbiu ya mchezo huo: HUYU NI WETU.