Kikosi cha Orlando Pirates kutoka Afrika Kusini, kimetua jijini Dar es Salaam tayari kwa mpambano mkali wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) dhidi ya wenyeji wao, Simba SC, unaotarajiwa kupigwa keshokutwa Jumapili.
Mchezo huo wa kwanza wa Kundi C utakaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru kuanzia saa 10:00 jioni, unatarajiwa kuwa wa upinzani mkali.
'The Buccaneers' wamewasili nchini wakitoka kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Golden Arrows siku ya Jumanne, matokeo yaliyowaimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi yao ya ndani ya Betway Premiership. P
Pirates wametua bila ya kiungo wao tegemeo, Thapelo Mokobodi, aliyepata majeraha kwenye mchezo huo akitarajiwa kukosa mchezo dhidi ya Simba.
Wakati Pirates wakitua, Simba iliingia kambini tangu juzi kukamilisha maandalizi ya mchezo huo ambao Wekundu wa Msimbazi wanahitaji ushindi.
Kikosi cha kocha Steve Barker kimepania kuendeleza rekodi ya ushindi wa asilimia 100 kwenye michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu kama walivyofanya kwenye ligi ya ndani.