Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Simba SC raia wa Senegal, Libasse Guèye, amefichua siri ya timu hiyo kuendelea kupata mfululizo wa ushindi msimu huu, akitaja mchango mkubwa wa kocha wa viungo pamoja na jopo la madaktari wa klabu hiyo.
Hatua hiyo inakuja huku klabu hiyo ikiwa imeweka rekodi ya kipekee kwa kushinda mechi zote 11 za mwanzo mfululizo kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/27, na kujichimbia kileleni mwa msimamo wakiwa na alama 33.
Akizungumza wakati wa Simba Media Day iliyofanyika jana, Guèye alieleza kuwa utimamu wa mwili na maandalizi mazuri ya kimwili ndiyo yanayowabeba uwanjani.
Alibainisha kuwa ushirikiano wa karibu kati ya idara ya matibabu na benchi la ufundi unahakikisha wachezaji wanabaki katika kiwango bora cha ushindani.
Mbali na siri hiyo ya ushindi, nyota huyo ambaye amekuwa kwenye kiwango bora (on-form) akihusika kwenye mabao 11 katika mechi 11 za Ligi Kuu akifunga mabao matatu na kutoa pasi za mabao (assists) nane, alifunguka kuhusu malengo yao makubwa msimu huu.
"Lengo langu kubwa na la klabu msimu huu ni kufika hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League)," alisema Guèye, huku kikosi hicho kikijiandaa na mchezo mzito wa hatua ya makundi dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Katika hatua nyingine, Guèye alitumia fursa hiyo kusimama kama ngao kwa mchezaji mwenzake, Ibrahim Doumbia, ambaye amekuwa akikosolewa na mashabiki.
Amewasihi mashabiki wa Simba kuacha kumshambulia na kumwekea presha kubwa kiungo huyo kwenye mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa Doumbia ni mpiganaji mkubwa anayejitolea kwa ajili ya timu.
Gueye pia ameeleza kuguswa na mapenzi ya mashabiki wa Msimbazi, akisema wimbo wa "Pige Kelele, Libasse Moto" unaoimbwa majukwaani umekuwa ukimpa motisha kubwa ya kupambana na kufanya vizuri kila anapokanyaga nyasi.