Zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Klabu ya Simba SC linatarajiwa kuhitimishwa rasmi leo, Ijumaa, Novemba 20, 2026, huku majina kadhaa maarufu yakijitokeza kuwania nafasi hizo.
Mchakato huo ulioanza Novemba 16, 2026, unasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), katika ofisi zake zilizopo Karume, jijini Dar es Salaam.
Hadi kufikia jana jioni, wanachama mbalimbali walikuwa wamejitokeza kuchukua fomu, huku nafasi ya Uenyekiti ikivuta hisia za wadau wa soka baada ya aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', kujitokeza kuwania nafasi hiyo.
Kujitokeza kwa Kaburu kumeongeza mvuto katika mchakato huo, huku macho ya Wanasimba yakielekezwa kwa wagombea wengine wanaoweza kuingia katika kinyang'anyiro hicho kabla ya muda kumalizika.
Katika nafasi za Ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, wanachama kadhaa wamejitokeza kuwania nafasi hizo, akiwemo Hassan Bakari Kakayoo, maarufu kama Mzee wa Salute, ambaye pia alichukua fomu ya kuwania nafasi hiyo mwaka 2022.
Wengine waliojitokeza ni Agness Daniel 'Aggy Simba', Mohamed Hamis 'Doctor Mo', Salum Hamidu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Matawi ya Simba Dar es Salaam, Eli Achahofu Paul Gongi, Christopher Kabalika Mwansasu, Wilfred Nyamwija, Said Tully na Anindumi Jonas.
Wakati zoezi hilo likielekea ukingoni, wadau wa soka wanaendelea kusubiri kuona iwapo Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Murtaza Mangungu, atajitokeza kuchukua fomu au kama kutakuwa na majina mengine makubwa yatakayoingia katika mchakato huo dakika za mwisho.
Kwa mujibu wa ratiba ya Kamati ya Uchaguzi, baada ya kufungwa kwa zoezi la leo jioni, hatua inayofuata itakuwa kutolewa kwa orodha ya awali ya waliochukua fomu, inayotarajiwa kuchapishwa kati ya Novemba 21 na 23, 2026.
Baada ya hapo, mchakato utaendelea katika hatua za mapingamizi na usaili kwa mujibu wa taratibu na kanuni za uchaguzi.
Uchaguzi huo ni sehemu ya mchakato wa kupata viongozi watakaoshiriki katika kuiongoza Simba SC katika kipindi kijacho, huku wanachama na mashabiki wakisubiri kufahamu majina yatakayokidhi vigezo vya kuendelea na kinyang'anyiro hicho.