Mwanachama maarufu wa Simba SC, Niva Lazaro Mmbaga, maarufu kwa jina la Mchungaji wa Simba, amejitosa rasmi katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya mwenyekiti wa klabu hiyo baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.
Mmbaga amesema hatua yake ya kuchukua fomu ni kutimiza ahadi aliyokuwa ameitangaza awali ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi ndani ya klabu ya Wekundu wa Msimbazi.
Akizungumzia uamuzi wake, Mchungaji huyo wa Simba amesema mbali na dhamira yake binafsi, amepata msukumo mkubwa kutoka kwa matawi mbalimbali ya Simba ambayo yanamuunga mkono katika safari yake ya kuwania uenyekiti.
Mmbaga ameeleza kuwa ana elimu inayomwezesha kugombea nafasi hiyo, huku akionyesha dhamira yake ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa klabu hiyo.
Aidha, amesema zipo sababu mbili za msingi zilizomsukuma kufanya uamuzi wa kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti, lakini ataziweka wazi na kuzifafanua kwa kina utakapofika wakati wa kampeni.
Kujitosa kwa Mchungaji wa Simba kunaongeza hamasa katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi hiyo, huku wanachama wakisubiri kusikia sera na mikakati ya wagombea kuhusu mustakabali wa klabu yao.