Barker haendi popote - Ahmed

Mwana Msimbazi By Mwana Msimbazi
β€’
13 Nov 2026
Barker haendi popote - Ahmed

Wanaotaka Steve Barker aondoke Simba SC huenda wakahitaji kusubiri kwa muda mrefu zaidi. Hayo ni baada ya Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, kuweka wazi msimamo wa klabu kuhusu hatma ya kocha huyo ambaye jina lake limeendelea kutikisa vichwa vya habari kufuatia tetesi za kuwindwa na vigogo wa soka la Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns.

Kila kukicha kumekuwa na taarifa zinazomhusisha Barker na uwezekano wa kurejea Afrika Kusini, huku baadhi ya taarifa zikimtaja kama mmoja wa makocha wanaoweza kuchukua nafasi ya Miguel Cardoso endapo Sundowns wataamua kufanya mabadiliko kwenye benchi lao la ufundi.

Lakini kwa upande wa Msimbazi, ujumbe ni mmoja tu: BARKER BADO YUPO SANA!

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally amesema Simba tayari imezungumza na kocha huyo kuhusu tetesi zinazozagaa na hakuna dalili zozote zinazoonyesha kwamba anataka kuondoka. Ameongeza kuwa klabu haijapokea ofa rasmi kutoka Mamelodi Sundowns.

"Tumezungumza naye na ametuambia hakuna jambo kama hilo. Kama mnavyojua, alikuwa Afrika Kusini kwa mapumziko mafupi, lakini amerudi Tanzania na kuanza mazoezi na timu," alisema Ahmed.

Tetesi za Barker kuwindwa na Mamelodi Sundowns zimeongezeka baada ya klabu hiyo ya Afrika Kusini kukabiliwa na sintofahamu kuhusu mustakabali wa kocha wake Miguel Cardoso.

Taarifa za vyombo vya habari vya Afrika Kusini zimemtaja Barker kama mmoja wa makocha wanaoweza kupewa nafasi hiyo kutokana na uzoefu wake mkubwa katika ligi ya nchi hiyo.

Barker si jina geni Afrika Kusini. Kabla ya kujiunga na Simba, alitumia takribani miaka tisa akiinoa Stellenbosch FC, ambako aliijenga timu hiyo kutoka kuwa ya daraja la chini hadi kuwa miongoni mwa timu zenye ushindani mkubwa.

Aliiongoza Stellenbosch kupanda Ligi Kuu mwaka 2019, akatwaa Carling Knockout mwaka 2023 na kuifikisha timu hiyo fainali za MTN8 mara mbili mfululizo mwaka 2024 na 2025.

Ni mafanikio yanayoeleza kwa nini jina lake limeendelea kuhusishwa na klabu kubwa.

SIMBA BADO INA MALENGO YA MUDA MREFU

Ukweli ni kwamba Simba haikumleta Barker Dar es Salaam kwa ajili ya kuja kupita na kuondoka baada ya muda mfupi.

Kocha huyo alijiunga na Msimbazi Desemba 2025 kwa mkataba wa miaka miwili akiwa na jukumu la kuijenga upya timu na kuifanya iwe na ushindani mkubwa ndani na nje ya Tanzania.

Na dalili za kazi yake zimeanza kuonekana. Simba imekuwa na mwanzo mzuri wa msimu wa 2026/2027, huku ikishinda mechi zote 10 za ligi kuu msimu huu.

Kwa sasa malengo ya Simba hayapo kwenye mafanikio ya ndani pekee. Klabu inataka kufanya vizuri zaidi Ligi ya Mabingwa Afrika na imeweka wazi matarajio ya kufika hatua ya nusu fainali.

Huo ndio mpango ambao Barker anatakiwa kuumaliza kabla ya kufikiria changamoto nyingine.

Simba SC Stories

Wagombea zaidi wajitokeza siku ya mwisho kuchukua fomu Simba
Wagombea zaidi wajitokeza siku ya mwisho kuchukua fomu Simba
9h ago
READ MORE β†’
Barker apania kuendeleza wimbi la ushindi baada ya mapumziko ya FIFA
Barker apania kuendeleza wimbi la ushindi baada ya mapumziko ya FIFA
14h ago
READ MORE β†’
Miquissone aibukia Singida BS, arejea tena Ligi Kuu Tanzania
Miquissone aibukia Singida BS, arejea tena Ligi Kuu Tanzania
17h ago
READ MORE β†’
Zoezi la kuchukua fomu Simba kuhitimishwa leo
Zoezi la kuchukua fomu Simba kuhitimishwa leo
17h ago
READ MORE β†’
Ligi Kuu inarejea leo baada ya mapumziko ya FIFA, Mnyama dimbani Jumamosi
Ligi Kuu inarejea leo baada ya mapumziko ya FIFA, Mnyama dimbani Jumamosi
19h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Ijumaa, Novemba 20 2026
Magazeti ya leo Ijumaa, Novemba 20 2026
22h ago
READ MORE β†’
Mchungaji wa Simba achukua fomu Uenyekiti wa Simba
Mchungaji wa Simba achukua fomu Uenyekiti wa Simba
1d ago
READ MORE β†’
Simba kinara wa mabao ya mipira ya kutenga ligi kuu
Simba kinara wa mabao ya mipira ya kutenga ligi kuu
1d ago
READ MORE β†’
Mpanzu, Chama, Oura jino kwa jino kuzifumania nyavu ligi kuu
Mpanzu, Chama, Oura jino kwa jino kuzifumania nyavu ligi kuu
1d ago
READ MORE β†’
Kapombe, Hamza, Nangu wamuongezea mzuka Barker
Kapombe, Hamza, Nangu wamuongezea mzuka Barker
1d ago
READ MORE β†’