Klabu ya Simba imethibitisha kumruhusu winga wake, Bakari Msimu, kuondoka nchini na kwenda Ubelgiji kwa ajili ya kufanya majaribio ya soka la kulipwa.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ameeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo umeamua kumpa nafasi mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 ili kumuwezesha kupambania ndoto zake za kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.
Winga huyo machachari alijiunga na Wekundu wa Msimbazi mwezi Julai mwaka huu akitokea klabu ya Coastal Union ya Tanga kwa mkataba wa miaka miwili.
Licha ya kutumika zaidi kama mchezaji wa akiba katika michezo ya hivi karibuni, kiwango na kipaji chake vimetosha kuvutia maskauti wa soka kutoka nchini Ubelgiji.
"Ni kweli Bakari Msimu amesafiri kwenda nchini Ubelgiji kwa ajili ya majaribio. Kama klabu, hatuwezi kuwa kikwazo kwa maendeleo ya wachezaji vijana pindi fursa kama hizi zinapojitokeza. Tunamtakia kila la heri na majaribio yakikamilika salama, taratibu nyingine za uhamisho zitafuata," alisema Ahmed Ally.