Wakati kikosi cha Simba kikirejea mazoezini baada ya mapumziko ya takribani wiki moja, beki kisiki wa timu hiyo Ismail Toure ataendelea kukosekana kutokana na jeraha la goti.
Hata hivyo habari njema kwa mashabiki wa Simba ni kuwa beki huyo huenda akauwahi mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ligi ya mabingwa dhidi ya Orlando Pirates utakaopigwa mwishoni mwa mwezi huu.
Toure tayari amekosa mchezo mmoja wa ligi kuu dhidi ya Namungo Fc taarifa za awali zikibainisha kuwa nje kwa takribani wiki tatu.
Beki huyo mrefu na mwenye utulivu mkubwa, amekuwa nguzo muhimu ya safu ya ulinzi ya Simba akiunda pacha ngumu ya Rushine de Reuck.
Toure, raia wa Ivory Coast mwenye umri wa miaka 28, alijiunga na Simba Januari 2026 akitokea FC Baniyas ya Falme za Kiarabu. Kabla ya hapo, aliwahi kuzitumikia timu za ASEC Mimosas, Marumo Gallants na Stellenbosch za Afrika Kusini.
Katika mechi kumi za Ligi Kuu Bara ambazo Simba imecheza msimu huu, Toure ameshiriki kwenye michezo tisa akianza katika kikosi cha kwanza. Katika michezo hiyo, amekusanya dakika 450 na kufunga mabao mawili.