Licha ya tetesi zinazomuhusisha Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker na klabu ya Mamelodi Sundowns, Simba haina mpango wa kumuachia kocha huyo, imefahamika.
Taarifa za uhakika ni kuwa uongozi wa Simba uko kwenye mchakato wa kumuongeza mkataba wa muda mrefu zaidi.
Hivi karibuni, klabu ya Mamelodi Sundowns iliripotiwa kummezea mate kocha huyo raia wa Afrika Kusini ili akachukue mikoba ya Miguel Cardoso, hatua iliyozua taharuki kubwa kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kutokana na kiwango bora ambacho timu hiyo imekuwa ikikionyesha tangu alipokabidhiwa kijiti mnamo Desemba 2025.
Hata hivyo, taarifa za ndani kutoka ndani ya klabu ya Simba zinasema kuwa hakuna uwezekano wowote wa Barker kuondoka kwa sasa.
Badala yake, mabosi wa Msimbazi wamejipanga kumpatia mkataba mpya wa muda mrefu utakaomfanya aendelee kusalia klabuni hapo na kujenga mradi endelevu wa soka la ushindani ndani na nje ya nchi.
"Barker bado yupo sana Msimbazi na anafurahia maisha ya hapa. Sundowns wanaweza kuwa wanamtaka kwa sababu ni kocha mkubwa, lakini ukweli ni kwamba hakuna uwezekano wa yeye kuondoka. Uongozi tayari upo kwenye mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya na mnono wa muda mrefu ili kulinda benchi letu la ufundi," kilieleza chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.
Kocha huyo ambaye mkataba wake wa awali utamalizika mwanzoni mwa 2027, ameirejesha Simba kwenye heshima iliyokuwa nayo misimu minne iliyopita sasa ikitawala soka la ndani mkakati ukiwa kufanya vyema zaidi kwenye ligi ya mabingwa pia.