Ushindani wa namba kwenye kikosi cha Simba SC umezidi kushika kasi, hali ikiwa ngumu kwa nahodha Shomari Kapombe ambaye tangu arejee kikosini imekuwa sio rahisi kwake kurejesha nafasi yake upande wa kulia.
Kapombe, ambaye amekuwa muhimili wa eneo hilo kwa miaka mingi, hivi sasa anapambana kurejea kwenye fomu yake ya kawaida baada ya kupona majeraha yaliyomweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Katika soka la ushindani, muda hausubiri; wakati mkongwe huyo akiwa wodini, Chilambo alipewa dhamana na ameitendea haki ipasavyo. Chilambo amewasha moto kwelikweli.
Beki huyo aliyetua Simba akitokea klabu ya Azam Fc, amekuwa na muendelezo mzuri wa kiwango (consistency), akionyesha ukomavu mkubwa katika kuzuia na uwezo mkubwa wa kupandisha mashambulizi.
Barker amempa Chilambo majukumu zaidi kwani anamtumia kwenye nafasi zaidi ya moja awapo uwanjani. Simba inapozuia hutumika kama beki wa kulia lakini inaposhambulia hutumika kama kiungo.
Umahiri wake huo umemfanya ajihakikishie nafasi mbele ya Barker huku pia akipewa majukumu makubwa zaidi kwenye timu ya Taifa.
Wakati Kapombe akihitaji dakika nyingi zaidi uwanjani ili kupata utulivu na 'match fitness' (utayari wa mchezo), kasi na fomu aliyonayo Chilambo hivi sasa inafanya iwe vigumu kumuweka benchi.
Ni wazi ushindani huo unamlazimisha Kapombe kuongeza juhudi kwenye uwanja wa mazoezi amshawishi Barker ampe nafasi.
Hata hivyo ni suala la muda tu, Wanasimba watamuona tena Kapombe uwanjani kutokana na wingi wa mashindano ambayo Simba inakwenda kukabiliana nayo katika kipindi kifupi kijacho.
Wakati hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa ikitarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi, michuano ya kombe la Shirikisho la CRDB nayo iko karibu kuanza.